Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako.
Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), limetangaza matokeo ya kidato cha sita kwa mwaka 2010 huku kiwango cha ufaulu kikionekana kushuka kwa asilimia 0.61 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa, shule zinazomilikiwa na serikali zimeibuka kidedea ambapo katika shule 10 bora zilizokuwa na watahiniwa zaidi ya 30, sita kati yake zinamilikiwa na Serikali wakati shule ya wasichana Marian ikiongoza kitaifa.
Aidha, kinyume na mwaka jana, wanafunzi wote 10 bora walioongoza kitaifa ni wavulana ambao wanatoka shule za Serikali wakati msichana aliyefanya vizuri anatoka shule ya Marian.
Kama ilivyokuwa kwa matokeo ya mwaka jana, shule za Zanzibar ndizo zilizoshika mkia ambapo shule tatu za mwisho kabisa zinatoka visiwani humo.
Aidha, matokeo ya watahiniwa 139 yamefutwa kutokana na kufanya udanganyifu wakati baraza limezuia matokeo ya watahiniwa 533 ambapo 484 kati yao hawajalipa ada ya mtihani na 49 hawakuwa na sifa.
Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako, alisema pamoja na kwamba wavulana wameongoza kitaifa, matokeo ya jumla yanaonyesha kuwa wasichana wamefaulu kuliko wavulana.
Alisema watahiniwa waliofanya mtihani huo walikuwa 63,434 ambapo watahiniwa 55,764 wamefanya vizuri.
Alisema wasichana 21,821 sawa na asilimia 90.39 wamefaulu kati ya wasichana 24,894 waliosajiliwa kufanya mtihani huo, wakati wavulana 33,943 sawa na asilimia 87.90 wamefaulu ikilinganishwa na 40,735 waliosajiliwa.
Alisema jumla ya watahiniwa 39,625 sawa na asilimia 82.17 wa shule wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu wakiwemo wasichana 15,650 na wavulana 23,975.
Aliwataja wanafunzi 10 bora na shule wanazotoka kwenye mabano kuwa ni Japhet John (Ilboru), Manyanda Chitimbo (Kibaha), Hassan Rajab (Minaki), Samuel Killewo (Feza Boys), Abdallah Taher (Mzumbe), Stivin Elias (Mzumbe), Paul Nolasco (Mzumbe), Alexander Marwa (Tabora Boys), Ephraim Swilla (Mzumbe) na Benedicto Nyato (Tabora Boys).
Wasichana waliofanya vizuri kwa mujibu wa Dk. Ndalichako na shule wanazotoka kwenye mabano ni Jackline Seni (Marian girls), Khadija Mahanga (Marian Girls), Cecilia Ngaiza (St. Joseph Ngarenaro), Esther Mlingwa (Marian Girls), Perpetua Lawi (Marian Girsl), Lilian Kakoko (Marian Girls), Gerida John (Dakawa), Subira Omary (Dakawa), Ruth Pendael (Morogoro) na Elaine Kijoti (Ashira).
Alizitaja shule 10 bora zenye watahiniwa zaidi ya 30 zilizofanya vizuri na mikoa zilipo kwenye mabano kuwa ni Marian Girls (Pwani), Mzumbe (Morogoro), Uru Seminari (Kilimanjaro), Kibaha (Pwani), Feza boys (DSM), Tabora Boys (Tabora), Tukuyu (Mbeya), Kifungilo (Tanga), Ilboru (Arusha) na Malangali (Iringa).
Katika kundi hilo, shule zilizoshika mkia ni High-View International (Unguja), Fidel Castro (Pemba), Sunni Madressa (Unguja), Neema Trust (DSM), Mtwara Technical (Mtwara), Muheza (Tanga), Tarakea (Kilimanjaro), Uweleni (Pemba), Modern (Arusha), Maswa Girls (Shinyanga).
Dk. Ndalichako alisema kuwa kwenye kundi la shule zenye watahiniwa chini ya 30, zilizoibuka kidedea ni Rubya Seminari (Kagera), Maua Seminari (Kilimanjaro), St. James Seminari (Kilimanjaro), St. Joseph Kilocha (Iringa), Dungunyi Seminari (Singida), Same Seminari (Kilimanjaro), Usongwe (Mbeya), St. Peter’s (Morogoro), Vituka (DSM), Vwawa (Mbeya).
Katika kundi hilo, Dk. Ndalichako alitaja 10 za mwisho kuwa ni Nkasi (Rukwa), Mt. Kilimanjaro (Kilimanjaro), Mbarali Preparatory (Unguja), Liliani Kibo (DSM), Ghomme (DSM) Adolec (Kagera), Mzizima (DSM), Dar es Salaam Christian Seminary (DSM), EDP Royal (DSM) na Sekei (Arusha).
“Baraza limesitisha matokeo ya watahiniwa 484 ambao hawajalipa ada lakini matokeo yao yatatolewa baada ya kulipa ada, 49 ya waliofanya mtihani wakiwa na sifa zenye utata wakati matokeo ya watahiniwa 139 yamefutwa baada ya kubainika kufanya udanganyifu ikiwemo kughushi vyeti,” alisema.
Alifafanua kuwa baraza hilo limebaini kwamba kulikuwa na udanganyifu ulioashiria watahiniwa kuonyeshana majibu na kuwa baraza limewaandikia wasimamizi wa vituo husika ili watoe maelezo kuhusiana na matukio hayo.
“Nina amini kwamba mamlaka za nidhamu wataangalia suala la mitihani kwa uzito wake na zitawachukulia hatua kali wahusika wote ili iwe fundisho kwa wengine,” alisema.
Kwa upande wa watahiniwa wa kujitegemea, Dk. Ndalichako alisema waliofaulu ni 10,457 sawa na asilimia 72.57 kati ya watahiniwa 14,643 waliofanya mtihani huo.
No comments:
Post a Comment