Wednesday, April 21, 2010

Dk. SLAA AIBWAGA SERIKALI


HATIMAYE Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (CHADEMA) ameibwaga serikali.

Ingawa ilikuwa imekana madai aliyotoa kuwa imechomeka kinyemela vipengele kwenye Muswada wa Sheria za Gharama za Uchaguzi uliosaniwa kwa mbwembwe kuwa sheria na Rais Jakaya Kikwete mwezi uliopita, juzi jioni iliurudisha bungeni ili kufanya marekebisho ya kuvinyofoa vipengele hivyo.

Muswada huo wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2010, ikiwemo Sheria ya Udhibiti wa Gharama za Uchaguzi, uliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema.

Werema ndiye aliyekuwa ameahidi awali, Dk. Slaa alipoibua hoja hiyo, kwamba kama serikali ingegundua kuwa vifungu hivyo vilichomekwa kinyemela, ingeomba radhi na kuurudisha muswada bungeni ufanyiwe marekebisho; ingawa baadaye alimbeza mbunge huyo, akajiingiza katika malumbano ya kutoa “ufafanuzi” wa kilichotokea, akasema vifungu viliongezwa ili kutafsiri kilichokuwa kimepitishwa na Bunge.

Lakini kitendo cha serikali kurejesha Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa ajili ya marekebisho bungeni, kimetafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya siasa nchini kuwa ni ushindi wa Dk. Slaa dhidi ya serikali.

Werema aliwasilisha muswada huo unaolenga kuzifanyia marekebisho sheria 16 zilizotungwa na Bunge, ikiwemo sheria namba 6 ya mwaka 2010.

Moja ya vipengele vilivyofanyiwa marekebisho ndani ya sheria hiyo, ni pamoja na kifungu cha timu ya mgombea kuhakikiwa na msajili wa vyama vya siasa, kilichokuwa kinalalamikiwa na Dk. Slaa. Sasa kimeondolewa.

Dk. Slaa katika madai yake, alikuwa amepinga kifungu hicho kwa madai kuwa kinakwenda kinyume cha misingi ya demokrasia, kwani timu za wagombea zingeweza kuondolewa kwa utashi wa msajili au ofisa mtendaji wa kata.

Akitetea uamuzi mpya wa serikali dhidi ya kauli yake ya awali, Werema alisema: “Kilichojitokeza bungeni kama inavyoonekana katika ‘Hansard’ (kumbukumbu za Bunge) ya Februari 11, 2010 kwa nia njema na kwa kuzingatia taaluma ya uandishi, tuliona kwamba kuidhinishwa kwa wajumbe wa timu ya kampeni ilikuwa ni jambo la kuzingatiwa.

“Baada ya kupata ushauri wa kamati ya uongozi kwa ushauri wa kamati mbili zilizoujadili muswada huu, sasa dhana ya kuidhinishwa kwa timu ya kampeni naomba iondolewe na badala yake wagombea wawasilishe orodha.”

Mapendekezo hayo yanahusu pia kuondoa ulazima wa mgombea kupata ridhaa ya msajili wa vyama vya siasa au ofisa mtendaji mkuu wa kata kuhusu gharama atakazotumia katika kampeni.

“Lakini pia mabadiliko haya yanagusa siku za kuhakiki na gharama za mgombea kupunguzwa kutoka saba hadi tano,” alisema Werema.

Msimamo mpya wa Werema unaunga mkono hoja mama ya Dk. Slaa kuhusu vifungu hivyo vya sheria. Hata hivyo, serikali haijaomba radhi kama alivyokuwa ameahidi mwanasheria huyo.

“Aidha inapendekezwa kufanya marekebisho katika kifungu cha 24 (1) kwa kupunguza siku ambazo kila chama cha siasa kitatakiwa kukamilisha mchakato wa uteuzi wa wagombea ndani ya vyama kutoka siku 21 hadi tano kwa lengo la kuainisha dhana ya siku iliyopo kifungu cha 9 (1),” alisema Werema.

Mbali na sheria hiyo, sheria nyingine zinazofanyiwa marekebisho ni ile ya Benki Kuu, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act) na Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.

Kwa upande wa sheria ya magazeti, mapendekezo ya muswada huo, yanalenga kuondoa ulazima wa kuwepo kwa washauri wa mahakama wakati wa kusikiliza mashauri ya kashfa za magazetini (defamation) na badala yake watakuwepo pale tu mahakama itakapoona ulazima.

Baadhi ya wabunge waliohojiwa na Tanzania Daima Jumatano, walisema kwa nyakati tofauti kuwa ndani ya mfumo wa serikali kuna kasoro nyingi.

Mbunge wa Kahama, James Lembeli (CCM), alisisitiza kuwa ndani ya mfumo wa serikali kuna kasoro nyingi, na akamtaka Rais Jakaya Kikwete kuwa makini nazo.

Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (CHADEMA), alisema hatua hiyo imeifedhehesha serikali ambayo ilikuwa imetamba, kwa kauli ya Werema, kwamba haijachomeka kipengele hicho kinyemela.

“Hii ni fedheha kubwa kwa serikali hii. Huu ni ushahidi tosha kwamba Dk. Slaa alikuwa sahihi wakati analalamikia vipengele hivi,” alisema Ndesamburo.

No comments:

Post a Comment