Na Ally Saleh
Maisha yote siasa za Zanzibar zinakuwa za changamoto kubwa. Hata juhudi gani zichukuliwe bado kuna pingamizi kadhaa wa kadhaa zitazozuka. Baadhi ni za kihistoria lakini baadhi yake ni za kuundwa undwa na kulazimisha lazimisha.
Hivi sasa Zanzibar inapita katika michakato kadhaa muhimu. Mmoja ni ule wa kuelekea kufanyika kwa Kura ya Maoni, wa pili ni ule wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa nne lakini mchakato mkubwa zaidi utaotokana na kufanikiwa kwa michakato hiyo miwili ni mchakato wa
kujenga Zanzibar Mpya.
Wako baadhi ya watu wanapinga michakato ya Kura ya Maoni na Uchaguzi Mkuu na kwa hivyo pia wanapinga pia fikra ya kujenga Zanzibar Mpya ambayo itaepuka siasa za chuki, hasama na kuviza maendeleo ya nchi bila sababu yoyote ile ya msingi zaidi ya kuendekeza mawazo mgando na ya kale na dhana za ubaguzi bila ya kujijua.
Wakati huu kukiwa na zoezi la uandikishaji wapiga kura katika Daftari la Kudumu (DKWK) upungufu kadhaa umekuwa ukijitokeza ambao huo tunaweza kusema ni wa kimuundo na kiutendaji na ambao tunao watu wa kuwaonyeshea kidole na kuamini kuwa wapo ambao wanaweza kuwajibika kuurekebisha.
Kwa mfano, ingawa Tume ya Uchaguzi imesema kuwa itaandikisha wapiga kura kwa raundi au awamu mbili tu, lakini imejitokeza wazi kuwa kuna watu wengi hawajapata fursa ya kujiandikisha kwa kosa lisilokuwa lao, kwa maana ya kuzembea.
Kwa inavyoelekea haitakuwa busara kabisa kwa Tume hiyo kuwa kichwa ngumu kukataa wapiga kura kwa maelfu, kwa sababu yoyote ile ikiwa kweli inataka kuhakikisha kuwa kunakuwa na uchaguzi huru hapa Zanzibar.
Na kwa hivyo akili yangu inanipa kuwa kutakuwa na raundi au awamu ndogo ya tatu. Katika awamu hii si lazima uandikishaji ufanywe jimbo kwa jimbo, lakini unaweza kufanywa katika ngazi ya Wilaya ili kila
mwenye haki apate haki hiyo kwa sababu haitaingia akilini uchaguzi unaofanywa Oktoba uandikishaji umalizikie mwezi wa Mei. Itakuwa dhulma kubwa.
Lakini pia tunaweza kunyooshea kidole taasisi ya Vitambulisho kunyima au kuchelewesha vitambulisho kwa wananchi kadhaa na fikra za taasisi hiyo kukataa kuwa kuna tatizo hilo ni sehemu kubwa ya tatizo la watu wengi pamoja na mke kukosa vitambulisho si kwa sababu ya uzembe lakini
kwa kushindwa kufanya kazi kwa mfumo wa kupata vitambulisho.
Siamini kuwa watu ambao watapata vitambulisho vyao kwa mfano leo, wakose haki ya kujiandikisha na hivyo kupiga kura kwa uchaguzi ambao utafanyika mwezi Oktoba. Itakuwa ni dhuluma kubwa, kwa sababu hawa
watakuwa ni kwa maelfu.
Ila matatizo mengine yanayohusu uandikishaji hayahusu Tume ya Uchaguzi wala taasisi ya Vitambulisono lakini zaidi ni ya wanasiasa na hawa hatuna nafasi ya kuwabana zaidi ya kuwasema hivi sasa kama tunataka kweli kuwa na uchaguzi huru hapa Zanzibar.
Mara nyingi huwa inasemwa juu ya suala la kupandikiza wapiga kura. Mara nyingi huwa pia inatajwa kuwa hili linafanywa na vyama vyote vya siasa. Lakini kuanzia sasa nimeanza kuwa na msimamo kuwa kwa hali ya
Zanzibar si rahisi hata kidogo kwa chama chochote chengine kisichokuwa CCM kupenyeza wapiga kura katika Daftari la Wapiga Kura.
Na kama chama chengine kisichokuwa CCM kinaweza kufanya hivyo basi ni kwa nafasi ndogo sana, kwa siri sana kinyume na inavyofanywa na CCM kwa wingi, kwa uwazi na kwa jeuri kubwa kabisa. Hali hii haionyeshi
kuwa kutakuwa na uchaguzi huru hapa Zanzibar.
Tuliona mwanzo wa zoezi hili la wapiga kura jinsi Chama cha Mapinduzi kilivyohusishwa na upandikizaji huko Pemba na hata hali hiyo kuikolezwa na utumaiji wa vitisho kwa kupelekwa vifaru na kimojawapo kikapinduka miguu juu.
Jeuri iliyofanywa mwishoni mwa wiki katika Mji Mkongwe na watu amboa kwa dalili zote walikuwa wakifanya hivyo kwa kinga ya CCM na vyombo vya dola, haiwezi kusaidia kabisa kuwa na uchaguzi huru hapa Zanzibar. Pia ni dhulma kubwa ya kisiasa na usaliti wa demokrasia.
Mkuu wa Polisi wa Mkoa aliarifiwa na Mbunge wa Mji Mkongwe na hata kulalamikiwa kuwa Polisi wanashiriki katika kuwapa nguvu wageni wa jimbo kupata fursa ya kuandikwa ilhali hawana haki.
Wazi na mchana kweupe wapiga kura waliletwa kuja kupandikizwa katika vituo vya Mji Mkongwe na bila ya kificho chochote waliletwa kwa magari na pia kuwekwa katika jengo la CCM la tawi lake pale Shangani. Hata
kuna gari la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar linalodaiwa kutumika kwa mujibu wa nambari zake.
Watu hawa waliletwa kwa magari pengine wakitokea mashamba lakini pengine pia wakitokea mitaa mengine kuja kujiandikisha ilhali wao wakijua na waliowaleta wakijua kuwa hawana haki ya kupiga kura katika jimbo hilo kwa sababu si wakaazi waliotimiza muda wa miaka mitatu
yaani miezi 36 kama sheria inavyosema.
Kwa mtu asiyejua mazingira na siasa za Zanzibar ataona hili haliwezekani. Kwani hakuna sheria, hakuna utaratibu au hakuna maafisa wa Tume? Vyote vipo lakini utekelezaji wake unaendeshwa kimatakwa na kwa hivyo Sheha ambaye ni afisa wa ngazi ya chini ya Serikali anavaa
jokho la CCM na anasimama kukataa wakaazi halali wasipige kura lakini anapitisha bila aibu wasiokuwa wakaazi kuandikishwa.
Mawakala wa vyama vya siasa wakati kama huu na katika mazingira ya kulazimisha wageni wa jimbo waandikishwe, huwa hawana haki ya kusema kitu na wale wanaothubutu wanatishwa, kondolewa kituoni na hata kukamatwa.
Pia mtu asiyejua siasa za Zanzibar atauliza CCM ipandikize wapiga kura Mji Mkongwe ili ipate nini? Ni kweli CCM inajua wazi wazi kuwa ina nafasi ndogo ya kulipata jimbo hilo kwa kura chache inazozipenyeza,lakini wadadisi wa siasa wanajua kuna lengo kubwa zaidi.
Lengo kubwa ni kulenga kupata wapiga kura wengi zaidi katika nafasi ya ugombezi wa Rais. Imeshuhudiwa katika chaguzi zilizopita wapiga kura wakipelekwa kwa magari kutoka kituo kimoja hadi chengine wakati wa upigaji kura na kwa hivyo kuongeza idadi ya wapiga kura kwa nafasi ya
Urais.
Kwa siasa Zanzibar husemwa “kichwa ndio muhimu” na kichwa ndio Urais ambapo vyama viko tayari kufanya lolote na zaidi kw aCCM ambayo haioti kabisa kuiachia nafasi hiyo na haiingia kabisa katika akili yao kuwa hilo linaweza kutokea.
Si kweli kuwa viongozi wa ngazi za juu wa CCM wala Serikali kuwa hawajui kinachoendelea na kama hawajui basi tuseme kuwa hawatimizi wajibu wao kama viongozi kwa sababu kama viongozi wanatakiwa wajue kinachotokea katika nchi.
Katika hali ya kuwepo Maridhiano ya kisiasa, mtu angetarajia kuwa Zanzibar itatupilia mbali vijisiasa vya kupandikiza wapiga kura,vijisiasa vya kuiba kura na vijisiasa vya kucheza na matokeo, wakati yote haya yameshaonekana yasipewe tena nafasi hapa Zanzibar, lakini
wapo watu bado wameganda katika mitizamo kama hiyo, ambapo naamini wanaungwa mkono na viongozi wenye sauti na maamuzi.
Sasa kama hali ni hii, hivi kweli tutarajie kuwa na uchaguzi huru ifikapo hapo Oktoba? Utakuwaje uchaguzi huru wakati kuanzia hivi leo wakaazi wa Mji Mkongwe wanajua hakika kuwa miongoni mwao wameandikishwa watu ambao si wakaazi wa jimbo hilo na kuwa watakuwa wapiga kura?
Jamani ninavyojua mie haramu haiji kwa matokeo tu, bali haramu inakuja toka katika mchakato. Na mchakato wa uchaguzi wa Zanzibar ushakuwa haramu toka mwanzo, uhalali wake utakuwepo kweli. Mimi siamini kabisa.
No comments:
Post a Comment