Wednesday, April 21, 2010

VYETI VYA NECTA KUWEKWA PICHA ZA MTAHINIWA


KUTOKANA na vitendo vya udanganyifu kukithiri kwenye vyeti vya kidato cha nne na cha sita, Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limeanza kuweka picha katika vyeti vya matokeo ya ngazi hizo za elimu, ili kuwawezesha wadau kumtambua mmiliki halali wa cheti.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza, aliliambia Bunge mjini Dodoma kuwa picha hizo huwekwa kwa kompyuta hivyo haziwezi kuondolewa kirahisi na mtu yeyote.

Uwekaji huo wa picha katika vyeti utaanza na vyeti vya watahiniwa waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2008 ambavyo vitachapwa Mei 2010.

Naibu Waziri huyo alisema hati za matokeo ya mitihani ya kidato cha nne 2009 nazo zimetolewa zikiwa na picha.

Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde, Dk Ali Tarab Ali (CUF), aliyehoji kwa nini vyeti vya kidato cha nne na sita visiwekwe picha ya mtahiniwa husika kwa kutumia kompyuta ili kuondoa tatizo la udanganyifu.

Mbunge huyo katika maelezo yake alidai baadhi ya vyeti vya matokeo ya mtihani wa kitaifa ya kidato cha nne na sita kutoka Necta, vinatumiwa na watu wengine wasio watahiniwa kwa ajili ya kutafuta ajira au nafasi za masomo nje.

Katika kujibu swali hilo, Mahiza alikiri kuwa ni kweli kwamba baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wamebainika kutumia vyeti vya matokeo ya mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne na sita visivyokuwa vyao, kwa ajili ya kutafuta ajira au nafasi za masomo ya juu, jambo ambalo ni kosa la jinai.

Alitoa mwito kwa wananchi wote kuacha mtindo wa kutumia vyeti visivyokuwa vyao kwani kufanya hivyo kunawanyima wenye vyeti stahili zao na ni kutenda kosa la jinai.

Katila swali lake la nyongeza, Mbunge huyo wa Konde alidai kuwa suala la mtu kutumia cheti ambacho sio chake mara nyingi linafanywa kwa makubaliano na mwenye cheti husika, hivyo alitaka kufahamu pia hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa wote walioshiriki kufanya udanganyifu huo.

Lakini kwenye majibu yake, Mahiza alisema kuwa kesi za kuuza cheti ni chache sana na mara nyingi kama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wanapata kesi za watu kupotolewa na huwa wanazipeleka Polisi ili zishughulikiwe.

No comments:

Post a Comment