Salma Said, Zanzibar
UCHAGUZI mkuu wa Zanzibar unatarajiwa kufanyika Oktoba 31 mwaka huu na matokeo ya uchaguzi huo, yatatangazwa kuanzia siku hiyo hadi Novemba 2 mwaka huu.
Jukumu la kutangazwa kwa matokeo hayo, kutafanywa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Hayo yamo katika taarifa ya Mwenyekiti wa tume hiyo, Khatibu Mwinyichande, iliyosambazwa kwa vyombo vya habari vya mjini Zanzibar.
Katika taarifa hiyo ya kurasa nne, Mwinyichande amesema mchakato wa kuandikisha wapiga kura wapya ulioambatana na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, ulianza Machi na kwamba utakoma itakapofika Mei 9 mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, shughuli hizo, zinahusu pia ubadilishaji wa shahada za zamani za kupigia kura.
Taarifa ilisema kukamilika kwa kazi hiyoo, kumetoa fursa kwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, kupanga tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu na masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi huo kwa mujibu wa katiba na sheria za uchaguzi ya mwaka 1984.
"Sheira ya mwaka 1984, kifungu cha 45(1)(a) inaeleza kuwa “endapo uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika, siku ya uteuzi kwa jimbo lolote halitokuwa chini ya siku tano au zaidi ya siku 25 baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wawakilishi," ilisema taarifa ikinukuu sheria.
Ilisema kwa msingi huo ZEC imezingatia ratiba za vikao vya mwisho vya Baraza la Wawakilishi na katika kupanga ratiba yake ya uchaguzi.
ZEC imesema uteuzi wa wagombea wa nafasi za urais, uwakilishi na udiwani utafanyika Novemba 9 mwaka huu.
“Uchukuaji wa fomu za urais wa Zanzibar utaanza tarehe 10/08 2010 na mwisho ni tarehe 30/08/2010. uchukuaji wa fomu za uwakilishi na udiwani utaanza tarehe 15/08/2010 na mwisho ni tarehe 30/08/2010 na pingamizi wa uteuzi zitafanyika tarehe 05/09/2010," ilisema taarifa ya ZEC
Kuhusu kampeni za uchaguzi huo, ZEC ilisema zitaanza Septembe 10 na kumalizika Oktoba 30 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment