WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Mohammed Seif Khatib amependekeza mgombea wa kiti cha urais atakayemrithi rais wa sasa Jakaya Kikwete, atoke visiwa vya Zanzibar.
Waziri Khatib alitoa pendekezo hilo jana, siku ambayo Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulikuwa unatimiza miaka 46 tangu waasisi wa mataifa haya mawili, Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume, walipotekeleza ndoto zao za kuungana.
Hata hivyo, Muungano huo unaonekana kuongezeka kasoro licha ya serikali kuweka vyombo vya kughulikia kupunguza kero zilizopo.
Waziri Khatibu, ambaye anatajwa kuwa kwenye kinyang'anyiro cha urais wa Zanzibar, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) kinachorushwa hewani kila siku kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 2:00 asubuhi.
Waziri huyo, ambaye hajakanusha tuhuma hizo akitaka watu wasubiri muda utakapofika, alisema jana kuwa kuwa katika kuongoza nchi, ni vema kukawa na utaratibu wa zamu baina ya Wazanzibari na Watanzania Bara unaotambulika kikatiba.
“Kwa sasa hatuna utaratibu huo wa kuongoza nchi kwa zamu, lakini ni vema tukawa na utaratibu huu wa kupokezana,” alisema Waziri Khatib bila kueleza hili litasaidia nini.
Kwa mujibu wa Khatib, katiba ya sasa imeweka zamu katika nafasi ya makamu wa rais pekee, ikieleza kuwa kama rais atatoka Tanzania Bara, makamu wake lazima atoke Zanzibar na kama atatoka Zanzibar, makamu atoke bara.
“Ni vizuri viongozi wetu wa kisiasa waliopo madarakani hivi sasa wakawaandaa vijana wazuri kwa ajili ya nafasi ya urais, ili muda ukifika tusipate tabu,” alisema Waziri Khatib.
“Pamoja na kwamba ni vema tukawa na zamu za kutawala nchi yetu, tuna kila sababu ya kuhakikisha tunapata viongozi wazuri, walioandaliwa na wenye uwezo wa kuongoza.”
Hadi sasa ni Ali Hassan Mwinyi, aliyeongoza serikali ya awamu ya pili, ndiye Mzanzibari pekee aliyewahi kuwa rais wa Serikali ya Muungano baada ya kuongoza nchi kutoka mwaka 1985 hadi 1995 wakati kulipofanyika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.
Waziri Khatib asema: “Ni jambo jema kuwa na zamu za kuongoza nchi baina ya pande mbili za Muungano, lakini hatulazimishi iwe hivyo kwa sababu halipo kikatiba kwa sasa.”
Alisema kwa sasa serikali inafuata katiba katika kupata wagombwea urais, lakini kama katiba itafanyiwa marekebisho leo na kuweka zamu za kuongoza nchi, basi serikali haina budi kufuata katiba hiyo.
“Kama katiba itafanyiwa marekebisho leo na kuweka utaratibu wa zamu wa kuongoza nchi basi sisi serikali na chama tutafuata katiba, lakini kwa sasa sual hilo halipo kikatiba,” alisema Waziri Khatib.
Waziri Khatib anaweza akawa waziri wa kwanza ndani ya serikali ya Muungano kutoa pendekezo la namna hiyo, ambalo kimsingi linaweza kuibua mjadala mpya.
Waziri Khatib pia alikiri kuwa kuna matukio mbalimbali yaliyosababishwa na kero za Muungano na hivyo kuutikisa, hata hivyo, alisema Muungano bado ni imara.
Akitaja matukio hayo, waziri Khatib alisema ni pamoja na lile la wabunge waliotaka serikali tatu, kundi lililojulikana kama G55 na kujiuzulu kwa aliyekuwa rais wa Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi, ambaye alikuwa makamu wa rais na makamu mwenyekiti wa CCM.
“Unajua Zanzibar ilipita katika kipindi cha vuguvugu la kisiasa na ikashutumiwa kuwa, mheshimiwa Aboud Jumbe alikuwa katika mpango wa kuanzisha serikali ya tatu ndani ya muungano, kwa hiyo baada ya kikao cha chama kilichofanyika CBE Dodoma, akasema anawajibika kwa kujiuzulu,” alisema Khatib.
“Lakini pia hatuwezi kusahahu malumbano na mijadala mikali ambayo ilihatarisha Muungano baina ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusu hoja ya hadhi ya Zanzibar na suala la mafuta,” aliongeza Waziri Khatib.
“Mtukio haya yalitikisa sana Muungano wetu, lakini tunashukuru pamoja na misukosuko hiyo bado muungano upo imara.”
Kuhusu utatuzi wa kero za Muungano, Khatib alisema wamefikia mahali pazuri na kwamba hadi sasa tayari mambo makubwa matatu yameshatafutiwa ufumbuzi.
“Moja ni Sheria ya Uvuvi ambayo makao makuu yake ni Zanzibar, biashara ya meli na Sheria ya Haki za Binadamu; haya ni mambo matatu makubwa katika kero za Muungano ambayo tumeyafanikisha,” alisema Waziri Khatib.
Hata hivyo alikiri kuwapo kwa kero nyingine nyingi, likiwemo suala la mgawanyo wa mapato na uchangiaji baina ya Bara na Visiwani.
Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema amesema utaratibu wa kupokezana uongozi kwa zamu si mbaya, lakini usiwekwe kikatiba.
“Tangu Muungano ulipoasisiwa, misingi tuliyowekewa na waasisio ni kupatikana marais kwa utamaduni wa mapenzi na makubaliano na sio kikatiba,” alisema Mrema.
Alisema Mwalimu Nyerere na Mzee Karume walikubaliana kwa mapenzi tu kwamba Nyerere awe rais na Karume awe makamo.
“Wala Karume hakusema kwamba awamu inayokuja mimi ndio niwe rais. Mimi nadhani ni utamaduni mzuri, tunaweza kupeana zamu za kuiongoza lakini isiwe kitu cha kikatiba,” alisema Mrema.
Alisema hatari ya kuweka utaratibu huo katika katiba ni uwezekano wa kupata viongozi wasio na uwezo na hivyo kusababisha migogoro ndani ya nchi.
“Nadhani waziri angesema kama kuna matatizo ya msingi katika Muungano, lakini tusitafute visingizio tu,” alisema Mrema.
Hata hivyo mwenyekiti Mwenza wa Mpango wa Utafiti wa Maendeleo ya Demokrasia nchini (REDET), Dk Benson Bana alisema wazo la Waziri Khatib si zuri kwa kuwa linaweza kuligawa taifa.
“Katika urais tunapima uwezo wa mtu na hatuangalii rangi, dini, kabila wa eneo la mtu. Tusijali mazingira anayotoka; tunaangalia ‘vision’ (dira) na uwezo wa mtu hata kama anatoka Pemba au Bukoba tunampa urais,” alisema Dk Bana.
“Hii ya waziri italigawa taifa, sisi sote ni Watanzania na tumeshatoka katika ubaguzi wa kikabila, kikanda, kidini na hata rangi wala hatuwezi tena kurudi nyuma tulikotoka,” aliongeza Dk Bana.
“Mimi nadhani inatosha hii ya kupokezana katika nafasi ya umakamu, yani kama rais atatoka bara makamu wake awe Mzanzibari na kama rais atatoka Zanzibar basi makamu wake atoke Tanzania Bara,” alisema Dk Bana.
No comments:
Post a Comment